Jumapili, 25 Agosti 2019

Njia 9 za Kutangaza Biashara Yako Bila Pesa

Matangazo ni swala muhimu kwa kila biashara. Tatizo linatokea pale ambapo biashara inashindwa kumudu gharama za matangazo, hasa matangazo ya gharama kubwa.
Naamini wewe kama mjasiriamali unafahamu kuwa kuna wakati bajeti ya biashara inakuwa imebana. Hivyo swala la kujitangaza linakuwa na changamoto.
Fuatilia makala hii kwa karibu ili nikufahamishe njia 9 unazoweza kuzitumia kutangaza biashara yako bure au kwa gharama nafuu sana.

1. Tumia tovuti

Tovuti au blog ni njia rahisi na ya gharama nafuu ya kujitangaza. Ikiwa una blog au tovuti ambayo inaidadi nzuri ya watembeleaji, unaweza kuweka tangazo la biashara yako hapo na likaonekana kwa watu wengi zaidi.

2. Tumia mitandao ya kijamii

Kama ilivyo wenye njia ya blog, vivyo hivyo unaweza kutumia mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Twitter, Instagram n.k. ili kujitangaza.
Kumbuka hivi leo karibu kila mtu anatumia mitandao ya kijamii. Hivyo kutangaza biashara yako kupitia kurasa au akaunti zako za mitandao hii ni rahisi na utawafikia watu wengi zaidi.

3. Tengeneza vifungashio au zawadi ndogo

Siyo lazima uwe na pesa nyingi ndipo utoe zawadi au huduma ya vifungashio vyenye chapa yako. Unaweza kubuni na kuchapisha vifungashio vyenye jina na maelezo mafupi kuhusu biashara yako ili kujitangaza.
Unaweza kutoa zawadi ndogo kama vile kalamu au shajara (diary) vyenye maelezo ya biashara yako.

4. Tengeneza kadi za kibiashara na vipeperushi

Unapopewa kadi ya kibiashara (business card) au kipeperushi lengo lake hasa ni kujitangaza. Unaweza kutengeneza kadi za kibiashara pamoja na vipeperushi vyenye maelezo mafupi kuhusu biashara yako.
Naamini njia hii ni nafuu sana kuliko kuweka tangazo kwenye televisheni wakati wa habari.

5. Kuwa wakala wa biashara kubwa

Kuwa wakala wa biashara kubwa ni njia moja nzuri ya kujitangaza na kuongeza wateja. Mara nyingi biashara kubwa huwatangaza mawakala wao katika matangazo yao ya gharama kubwa.
Hivyo, kwa kuwa wakala wa biashara au kampuni kubwa kama vile makampuni ya simu, bima, dawa, pembejeo, au fedha; utakuwa umepata nafasi ya kutangazwa bure kabisa.

6. Hudhuria semina na makongamano

Njia nyingine nzuri na rahisi ya kujitangaza ni kwa kuhudhuria semina, makongamano au sehemu zenye mikusanyiko.
Uwapo katika maeneo haya, hakikisha unatafuta angalau nafasi ya kutoa salamu katika maeneo haya, ukipewa nafasi ya kuzungumza taja tu hata jina la biashara yako kwani ina maana kubwa sana. Unaweza kuvaa pia mavazi yenye maelezo au matangazo ya biashara yako.

7. Jitolee au toa misaada

Naamini mara kadhaa umewahi kuona wafanyakazi wa kampuni au biashara fulani wakitoa misaada au hata kujitolea kufanya kazi kama vile usafi wa mazingira.
“Hakuna chakula cha bure kwenye uchumi.”
Je ni nini hasa msingi wa swala hili? Kama wanauchumi wa kale walivyotangulia kusema kuwa hakuna chakula cha bure kwenye uchumi, vivyo hivyo matendo ya kujitolea au msaada yana lengo fulani.
Mara nyingi makampuni au biashara fulani zinapotoa misaada waandishi wa habari hurekodi na kutangaza habari hiyo. Hii ni njia nzuri sana ya kujitangaza.

8. Endesha shindano

Nani asiyependa kushinda? Naamini hata wewe unapenda kushinda zawadi fulani.
Ili ushinde unatakiwa kununua bidhaa au kusambaza habari kuhusu biashara fulani, je kwa njia hii hujaitangaza biashara hiyo? Naamini utakuwa umefanya hivyo tayari.
Unaweza kuendesha shindano dogo lenye zawadi za kawaida kama vile mikoba, vocha za simu, vinywaji, kalamu au hata bidhaa unazouza. Kwa njia hii utajitagaza kwa gharama nafuu kabisa.

9. Toa elimu au ushauri bure

Kama kuna elimu au ushauri fulani unaoweza kuutoa ambao unaendana na biashara yako; fanya hivyo sasa.
Kwa njia hii utafahamika na kuwafikia watu wengi zaidi na hivyo kuitangaza biashara au huduma yako kwa urahisi na  kwa gharama nafuu kabisa.
Hitimisho
Kufanikiwa katika kitu chochote kunahitaji mikakati sahihi na ubunifu. Naamini umeona jinsi ambavyo unaweza kutumia njia mbalimbali kujitangaza kwa bei nafuu au bure kabisa.
Naamini hutoumiza tena kichwa kufikiri njia za kupata pesa nyingi kwa ajili ya matangazo ya gharama kubwa.

Jinsi ya Kuanza Biashara na Mtaji Mdogo

Watu wengi wamekuwa wakitamani kuanza biashara lakini wanafikiri namna ya kuanza kwani mtaji wao ni mdogo sana.
Usiogope; kuwa na mtaji mdogo au kutokuwa nao kabisa sio mwisho wako wa kutimiza malengo yako.
“Usilie juu ya kile ambacho huna; tumia vizuri kile ulichonacho.”
Reginald Mengi
Zipo mbinu mbalimbali ambazo zinaweza kukuwezesha kufanya biashara hata kama utakuwa na mtaji mdogo. Tafadhali fuatilia hoja jadiliwa hapo chini kwa ufafanuzi zaidi.

1. Kuwa mbunifu

Moja kati ya mambo ambayo yatakusaidia sana kwenye kuanza biashara kwa mtaji mdogo ni ubunifu. Kwa njia ya ubunifu utaweza kushinda biashara na bidhaa zilizoko sokoni kwa urahisi zaidi. Unaweza kufanya haya yafuatayo:
  • Chagua wazo la biashara unalolipenda na kuliweza vyema. Hili litakusaidia kukabili changamoto vyema.
  • Angalia tatizo au uhitaji uliopo sasa na uutatue kwa bidhaa au huduma yako.
  • Panga bei vizuri; unaweza kuweka bei ambayo ni tofauti kidogo na bidhaa au huduma ambazo tayari ziko sokoni ili uwavutie wateja.
Kwa kufanya mambo yaliyoelezwa hapa juu utaweza kukuza biashara na mtaji wako kwa muda mfupi zaidi.

2. Anza na unachokijua

Unapokuwa na mtaji mdogo huhitaji kuhusisha mambo mengi mageni au yanayotegemea sana watu wengine kwa kuwa huna pesa za kuyagaramia.
Kwa mfano kama unaanzisha biashara ya ushonaji basi anza kutengeneza mavazi yale unayoyaweza kwa kutumia vifaa ulivyonavyo; kwa njia hii utajenga mtaji wako kisha baadaye utaweza kuajiri wengine watakao kuwezesha kutengeneza aina nyingine zaidi.
Unapofanya kile unachokijua gharama huwa haziwi kubwa sana kwani ni kitu unachokimudu mwenyewe.

3. Waambie watu unachokifanya

Waambie watu unachokifanya kwani hili litakuwezesha kupata wateja na kufahamika. Watu wakijua unachokifanya watatamani kukifahamu zaidi; hili litakuwezesha kupata wateja na kuongeza mtaji wako.
Usiogope kueleza kuwa unafanya biashara ya mboga, chakula, duka dogo la bidhaa n.k. Kwani hujui unaemweleza atakuwa nani kwenye biashara yako.
Ukiwa na marafiki kwenye mitandao ya kijamii waeleze pia juu ya kile unachokifanya.

4. Epuka gharama zisizokuwa za lazima

Kwakuwa bado una mtaji mdogo jitahidi kuepuka garama zisizo za lazima kama vile ofisi ya kifahari, matangazo ya gharama kubwa n.k.
Kuwa na matumizi mazuri ya fedha hasa kwa mambo ya msingi tu. Watu wengi wameshindwa kwenye biashara kwa sababu wameanza biashara kwa mbwembwe za matumizi badala ya huduma bora zenye ubunifu.

5. Fanya kazi kwa bidii

Kamwe huwezi kuona mafanikio kama hutofanya bidii. Kumbuka wewe ni mjasiriamali anayeanza hivyo ni lazima ufanye bidii ili soko litambue kuwa upo pia unaweza.
Tumia muda vizuri, pia hakikisha unatoa huduma yenye ubora wa hali ya juu kwa bei ambayo wateja wataweza kuimudu. Jitese kwa muda mfupi kwa kipindi cha kuweka msingi wa biashara yako kwani hata kipindi cha kupanda katika kilimo huwa ni cha taabu.

6. Tumia rasilimali na fursa zilizopo

Njia nyingine itakayokuwezesha kuanza biashara ukiwa na mtaji mdogo ni kutumia fursa zilizopo. Kumbuka kuwa huwezi kutengeneza fursa kama huwezi kutumia fursa zilizopo.
Tumia fursa kama vile mitandao ya kijamii ili kujitangaza. Pia unaweza kutumia udhaifu uliopo katika biashara nyingine za watangulizi wako kama fursa kwani unaweza ukarekebisha udhaifu huo kupitia biashara yako.
Zipo pia fursa za mikopo yenye masharti nafuu ambayo itakuwezesha kuongeza mtaji wako. Kumbuka unahitaji kutumia mkopo kwa makini kwani utahitajika kuurudisha pamoja na riba tena kwa wakati.

7. Jali wateja

Kujali wateja katika biashara  ni jambo muhimu sana kama unataka kuona matokeo chanya. Siku zote ninapenda kusema “wateja hufugwa”. Wateja hufugwaje? Hufugwa kwa huduma nzuri.
Waheshimu wateja wako pia hakikisha unatimiza na kumaliza haja zao katika ubora wa hali ya juu. Kumbuka siku zote mteja huja kwanza kabla ya pesa; hivyo usitangulize pesa kabla ya huduma nzuri kwa mteja.
Ukilifanyia kazi hili utaweza kukuza biashara na mtaji wako kwa muda mfupi.

Hitimisho
Zilizojadiliwa hapa ni mbinu saba zitakazokuwezesha kuanza biashara na mtaji mdogo. Usiogope unaweza hata kama una kiasi kidogo sana cha fedha.
Thubutu, nza, fanya bidii, weka nidhamu, mtangulize Mungu na hakika utaona mafanikio chanya katika biashara yako.
“Anzia ulipo.Tumia ulicho nacho. Fanya unachoweza.”
Arthur Ashe

Mbinu 10 za Kuongeza au Kuvutia Wateja Kwenye Biashara

Haijalishi huduma au bidhaa yako ni kubwa kiasi gani, biashara yako haitazalisha pesa kama wateja hawatakuwa tayari kununua bidhaa au huduma yako. Hakuna wateja, hakuna biashara.
Tatizo la kukosa wateja hukabili sana biashara ndogo, na hata kusababisha biashara hizo kufa. Siyo kwamba wateja hawapendi kununua bidhaa za biashara hizi, bali tatizo kubwa ni mbinu duni za kujitangaza na masoko.
Katika makala hii nitakueleza mbinu 10 rahisi na za gharama nafuu ambazo unaweza kuzitekeleza na ukaongeza au kuvutia wateja zaidi kwenye biashara yako.

1. Lugha nzuri

Katika mambo yanayowapotezea wafanyabiashara wengi wateja ni lugha mbaya kwa wateja. Hakuna mteja anayependa kupokelewa au kujibiwa vibaya.
Hakikisha unazungumza na wateja wako kwa namna bora ambayo wataona unawajali, unawathamini na kuwaheshimu.
Mimi mwenyewe ninapenda kwenda kwenye biashara ambayo wahusika wana lugha nzuri; huwa nawashauri pia rafiki zangu kwenda kwenye biashara za aina hiyo. Hivyo hakikisha unatumia mbinu hii ili kuongeza wateja.

2. Huduma au bidhaa za bure

Wateja wengi wanapenda vitu vya bure au zawadi. Siyo lazima ufanye jambo kubwa la bure ili kuwavutia wateja; hata jambo dogo tu linaweza kuwavutia sana.
Ili kuwavutia wateja unaweza kutoa huduma au vitu vya bure kama vile kalamu, mifuko, shajara (diary) au hata maji ya kunywa. Kwa njia hii utawavutia wateja wengi zaidi.

3. Punguzo

Punguzo ni njia bora sana ya kukabiliana na ushindani wa kibiashara na kupata wateja. Ikiwa mwenzako anauza sabuni kwa shilingi 2,100, wewe uza 2,050. Unaweza usipate faida kubwa kwenye bidhaa moja lakini utapata faida kubwa kwenye mauzo ya jumla.
Kwa mfano ikiwa faida kwenye sabuni hapo juu ni sh. 100, muuzaji wa kwanza akauza sabuni 5 kwa sh. 2,100 atapata faida ya sh. 500.
Lakini wewe ukauza sabuni 20 kwa sh. 2,050 utapata faida ya sh. 1,000. Je huoni kuwa umeuza na kupata faida zaidi kutokana na kuvutia wateja wengi kupitia punguzo? Weka punguzo sasa.

4. Shindano

Siyo lazima uwe na pesa nyingi ndipo uweze kuendesha shindano. Unaweza kuendesha shindano lenye zawadi ndogo kama vile vocha, kalamu, mikoba, shajara au hata vinywaji.
Kwa njia ya kuweka shindano watu wengi watavutiwa kununua bidhaa au huduma zako ili wawe washindi. Unaweza pia kuweka bidhaa au huduma zako kama kitu cha kushindaniwa badala ya zawadi nyingine.

5. Anzisha tovuti au blog

Watu wengi hawafahamu umuhimu wa tovuti au blog. Wengi hufikiri kuwa ni mahali pakuweka matangazo ya watu wengine ili wakulipe.
Ukweli ni kuwa blog au tovuti ni muhimu sana kwa ajili ya kuongeza wateja kwa njia ya kutangaza biashara yako.
Ukiwa una blog nzuri yenye watembeleaji wa kutosha, unaweza kuitumia kutangaza na kuuza bidhaa zako wewe mwenyewe na ukajipatia pesa nyingi.

6. Tumia mitandao ya kijamii

Kama ilivyo kwa blog na tovuti, vivyo hivyo mitandao ya kijamii inaweza kutumiwa kuzalisha pesa nyingi.
Ikiwa unataka kuongeza wateja, basi wafahamishe watu kupitia mitandao ya kijamii juu ya huduma au bidhaa zako. Hakikisha wanazielewa na kuweza kuzifikia kwa urahisi.

7. Matangazo

“Biashara ni matangazo.”
Biashara nyingi hupuuza nafasi ya kujitangaza ili kuongeza wateja na hatimae kupata faida zaidi. Siyo lazima utumie njia za gharama kubwa kujitangaza kwani zipo njia nyingi sana.
Unaweza kutumia mitandao (rejea mbinu ya 5 na 6), vifungashio, saini ya barua pepe (email signature), card ya utambulisho wa biashara (busness card), vipeperushi n.k.

8. Toa misaada

Je umeshawahi kujiuliza kwanini biashara na kampuni nyingi hutoa misaada mbalimbali? Je ni kwa kuwa wana pesa za ziada au wanawapenda sana wale wanaowasaidia?
Ni wazi kuwa hii ni mbinu nzuri sana ya kujitangaza na wala si vinginevyo. Kwa njia ya kutoa misaada wateja huongezeka zaidi kwani watu huifaahamu biashara husika, pia huichukulia kama biashara inayowajali zaidi.
Kumbuka siyo lazima utoe misaada mikubwa au ya pesa nyingi. Unaweza kutoa hata bidhaa zako au huduma yako kama msaada kwa watu au taasisi fulani.

9. Lenga changamoto

Watu wananunua bidhaa au huduma fulani ili itatue changamoto zao. Hivyo kuendesha biashara isiyolenga changamoto za wateja haitapata soko.
Hebu fikiri mtu anaanzisha duka la kuuza dawa za Ebola Kenya au Tanzania, je atapata wateja kweli? Ni wazi kuwa hatapata wateja kwani tatizo la Ebola kwa Tanzania na Kenya ni dogo sana.
Hivyo ili kuongeza wateja hakikisha unakuwa mbunifu na kulenga changamoto na mahitaji ya wateja.

10. Shirikiana na biashara au kampuni kubwa

Hebu fikiri kampuni kama Vodacom au Airtel wakikutaja kwenye matangazo yao kuwa wewe ni wakala wao; je unafahamu ni nini kitatokea? Moja kwa moja utafahamika zaidi pamoja na kile unachokifanya na utaongeza wateja zaidi.
Kumbuka kushirikiana na kampuni au biashara nyingine kubwa hukufanya pia uaminike zaidi kwa wateja.